Articles on political party manifestos coming soon in IsiZulu and English. Yazi ngaphambi kokuba uvote!
Picha ya Wangari Maathai: The Guardian
Iliyoandikwa na Esther Johnson
Iliyochapishwa Aprili 24, 2026
Wangari Maathai alikuwa shujaa wa mazingira wa Kenya aliyefundisha kuwa mbegu moja inaweza kuokoa misitu na kubadilisha historia. Alizaliwa mwaka 1940 katika kijiji cha Ihithe, Nyeri, ambapo alikua akicheza chini ya miti mikubwa ya mitini(fig trees), miti ambayo aliamini ilikuwa mitakatifu Baada ya kusoma biolojia nchini Marekani na kuwa mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki kupata shahada ya uzamivu (PHD), alirudi Kenya na kushtushwa na kasi ya uharibifu wa mazingira.
Mwaka 1977, alianzisha harakati ya Green Belt Movement. Wangari aliona kuwa ukataji wa misitu ulikuwa ukisababisha mito kukauka na njaa vijijini. Alianza na wanawake wachache, akiwafundisha kupanda miti ya asili kama Muringa (Moringa), Mukuyu (Sycamore Fig), na Mvule (African Teak/ Iroko). Tofauti na miti ya kigeni, miti hii ya asili ililinda udongo na vyanzo vya maji. Wangari alitembea vijijini akitoa mafunzo ya vitendo: "Chimba shimo kubwa mara mbili ya ukubwa wa mizizi, mwagilia maji kila siku, na uulinde mti dhidhi ya mbuzi." Kwa kila mti ulioishi, wanawake walipata malipo kidogo, jambo lililowapa uwezo wa kiuchumi na heshima katika jamii zao.
Harakati za Wangari hazikuwa za mazingira pekee, bali pia za haki za kijamii. Mwaka 1989, aliongoza mapambano dhidi ya mpango wa serikali wa kujenga jengo la ghorofa 60 katikati ya Bustani ya Uhuru (Uhuru Park), ambayo ni mapafu ya jiji la Nairobi. Licha ya kupingwa na kukamatwa na polisi, msimamo wake thabiti ulifanya wawekezaji wajitoe na bustani hiyo ikasalia kwa ajili ya umma. Vilevile, mwaka 1999, alinusuru Msitu wa Karura dhidi ya unyakuzi wa ardhi. Alikabiliana na tingatinga (bulldozers) akiwa na mche wa mti mkononi, akisisisitiza kuwa mazingira hayawezi kuuzwa kwa ajili ya faida ya wachache.
Kufikia mwaka 2004, Green Belt Movement ilikuwa imepanda takriban miti milioni 30. Mwaka huo huo, Wangari Maathai aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza Mwafrika kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel. Kamati ya Nobel ilitambua mchango wake katika kuunganisha utunzaji wa mazingira, demokrasia, na amani. Aisema: "Miti ni alama ya amani; tunapopigana juu ya rasilimali zinazopotea, amani hutoweka." Wangari alifariki mwaka 2011, lakini urithi wake unaendelea. Leo hii, Kenya imeweka malengo makubwa ya kupanda mabilioni ya miti, ikiwa ni mwendelezo wa ndoto ya binti huyu wa Nyeri aliyemini kuwa mabadiliko huanza na mbegu moja.